SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inafanya marekebisho ya katiba ya mwaka 1984, ambayo yanaipa Zanzibar hadhi kamili kama nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Marekebisho hayo ya katiba yanatarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoanza leo Zanzibar, ambapo pia yataruhusu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa rasimu ya marekebisho ya katiba hiyo, sura ya kwanza ibara ya kwanza iliyokuwa ikisomeka, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefutwa chini ya marekebisho hayo.
Rasimu hiyo ambayo itawasilishwa na Mwanasheria Mkuu, Idd Pandu Hassan, inapendekeza kifungu hicho sasa kisomeke ‘Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguuka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliitwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar’.
Aidha, marekebisho hayo ya katiba yamegusa kifungu cha pili na kueleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Marekebisho hayo pia yamegusa mamlaka ya rais katika kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Kabla ya marekebisho hayo kifungu cha pili cha Katiba ya Zanzibar kilikuwa kikisomeka ‘kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za serikali, Rais wa Jamhuri ya Muungano akishauriana na rais anaweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa’.
Kwa habari zaidi ingia humu