Jinsi ya Kuagiza Gari Nje ya Nchi kama Japan Bila Kutapeliwa (Hatua Zote)

Kwenye hii makala ntakueleza namna ya kuagiza magari mazuri kwa bei poa nje ya nchi kama Japan, UK, Singapore, Hongkong, Dubai na nchi nyingine kupitia mitandao mbalimbali bila ya kutapeliwa au kupokea gari bovu.

Hapa natazungumzia zaidi uagizaji wa magari yaliyotumika au kuwa na mmiliki mmoja wa kwanza (used au second hand cars).

Ntakueleza namna ya kuagiza gari au magari kutoka nje ya nchi kwa usalama na labda ukafanya kuwa ndo biashara yako.

Ntatumia mfano wa Toyota Raum niliyoiagizaga kutoka Beforward.

Mimi nafanya biashara ya kuuza magari na pia nasaidia watu kununua magari ambayo hayapo kwenye show room yangu au ata ambayo yapo nasaidia pia.

Ntakuonyesha hatua zote unazotakiwa kuzifwata na tunazozitumia kuagiza magari kwa ajili ya show room yetu na wateja wetu.

Mara nyingi bei za magari yaliyopo online zipo chini sana kulinganisha na bei zilizopo kwenye mashow room Tanzania, pia machaguo ya magari ni mengi kulingana na yale yaliyopo show room.

Ukiweza kuagiza gari online utaweza kukidhi mahitaji yako mbalimbali ya kibinafsi na ya kibiashara.

Ili uweze kununua gari kwa usalama inabidi kufuata hatua zifuatazo:

 • Kuchagua gari kutoka kwenye website salama
 • Vigezo muhimu vya gari yako ambavyo vitachangia kujua kiasi cha kodi ya TRA na ushuru wa Forodha
 • Tathimini ya kodi na ushuru bandarini kabla hujalipia gari (MUHIMU)
 • Kulipia bei ya gari kwa muuzaji
 • Usafirishaji wa gari kwenda bandari karibu na wewe
 • Kupokea gari na kulipia kodi ya TRA na ushuru

Hatua #1: Kuchagua gari kutoka kwenye website au soko salama

Hapa kuna aina mbili za uchaguzi:

 • Kutoka katika website za kampuni za kuuza magari
 •  Kutoka katika soko la magari

Utahitajika kufungua akaunti katika websites hizi ili uweze kuanza kuzitumia kikamilifu.

Uchaguzi wa magari kutoka kwenye website ya kampuni za kuuza magari

Wakati nanunua gari langu la kwanza niliagiza moja kwa moja kupitia mtandao wa Beforward. Kipindi bado hawajafungua ofisi Tanzania.

Gari yangu ya kwanza Toyota Raum

Ilikuwa rahisi kwa mimi kufanya maamuzi hayo kwasababu nlikuwa tayari nina marafiki ambao walikuwa wameshewatumia Beforward kuagiza magari.

Hii ni njia rahisi ya kufwata, kuepusha website tapeli. Unaagiza kwenye kampuni iliyo na rekodi nzuri na iliyotumiwa na ndugu, jamaa na marafiki.

Uchaguzi wa magari kutoka kwenye soko la magari

Soko la magari linakuwa na taarifa za makampuni mbalimbali ya magari zikiambatana na picha za magari waliyokuwa nao.

Mojawapo ya soko maarufu na tunalolitumia mara kwa mara ni Tradecarview.

Uzuri wa kununua gari katika soko ni kwamba kunakuwa na machaguo mengi zaidi ya magari,bei pia mara nyingi zinakuwa za ushindani.

Pia utapata maoni ya wanunuzi waliopita kuhusu huduma na ubora wa magari ya kampuni fulani.

Pia masoko aya yanakuwa na huduma ya “Escrow” ili kulinda usalama wa fedha za mteja .

Kwa mfano ukitaka kununua gari Tradecarview, ukishachagua gari pamoja na bandari litakalofikia, invoice utakayopewa utawalipa tradecarview 100%.

Tradecarview watakaa na hela yako bila kumpa muuzaji mpaka pale muuzaji atakapokutumia “B/L- Bill of Lading”. Hii B/L ni document inayotoka kwa msafirishaji ikiwa na taarifa za kitu kinachosafirishwa anayopewa mwenye mzigo (muuzaji).

Tradecarview watampa muuzaji hela akishaonyesha B/L na kuhakikisha gari imetumwa.

Pia tradecarview wanaweza kukurudishia hela yako iwapo muuzaji akishindwa kutuma gari katika mda mliokubaliana, au muuzaji hakipata matatizo ya kiufundi au kiofisi akashindwa kukutumia gari.

Hatua #2:Vigezo muhimu vya gari yako ambavyo vitachangia kujua kiasi cha kodi

Ukisha amua website gani utatumia kununua gari, sasa inabidi kuchagua gari kulingana na matakwa na mapenzi yako.

Ila wakati unachagua gari usiangalie tu bei kuna vitu muhimu inabidi pia uvifikirie kwenye kufanya maamuzi.

 • Upatikanaji wa vipuri na bei za vipuri Tanzania
 • Ukubwa wa engine (CC) na ulaji wake wa mafuta (Hii itachangia kujua kiasi cha kodi pia. Hatua #3)
 • Aina ya mafuta (Petroli au Diesel)
 • Mwaka gari lililotengenezwa (Hii itachangia kujua kiasi cha kodi pia. Hatua #3)
 • Je gari lilipata ajali kabla?
 • Je ni LHD au RHD?
 • Kilometre gari lilizotembea
 • Bei ya gari, usafirishaji, insurance pamoja na ukaguzi
 • Je gari ni manual au automatic, lina 4-Wheel Drive au lah

Kama hauna ufahamu na hivi vitu ni vizuri ukaomba ushauri kutoka kwa watu wenye uzoefu na magari.

Upatikanaji wa vipuri na bei za vipuri Tanzania

Wakati unanunua gari pia inabidi uangalie upatikanaji wa vipuri. Magari yanahitaji matunzo na kubadili vipuri. Kimsingi kama una uwezo mzuri wa kifedha kupata vipuri si tatizo unaweza agiza toka sehemu yeyote duniani.

Sisi tunatoa huduma ya kusaidia watu kuagiza vipuri visivyopatikana Tanzania.

Ukubwa wa engine (CC) na ulaji wake wa mafuta (Engine Size)

Pia lazima uangalie ukubwa wa Engine na ulaji wake wa mafuta. Kuna magari yanakula zaidi mafuta zaidi ya mengine. Na mengine yananguvu zaidi ya mingine kama kupanda milima mikali au kubeba mizigo.

Ukubwa wa Engine una mahusiano ya moja kwa moja na kiasi cha kodi utakacholipa. Tutazungumzua ulipaji kodi katika hatua #3.

Aina ya mafuta (Petroli au Diesel)

Aina ya mafuta gari yako itakayotumia na upatikaniji wa mafuta ayo katika eneo uhusika gari litakalo tumika. Nalo ni jambo la kuangalia.

Mwaka gari lililotengenezwa

Mwaka wa gari uliotengenezwa hili ni jambo litakalochangia sana kwenye ulipaji wa kodi. Serikali ina sera ya kuzuia vitu chakavu kuingia nchini kwahiyo imeweka kiwango kikubwa cha kodi kwa magari makuu yaliyo chakaa . (Hatua #3)

Je gari lilipata ajali kabla?

Hili ni swala la msingi sana kumuuliza muuzaji. Maana kuna wauzaji si waaminifu, wanaweza kukuuzia gari iliyopata ajali kwa bei sawa na gari nzima au kukuuzia bila kukutaarifu.

Je ni LHD au RHD?

Je gari unalotaka kununua ni Left Hand Drive (LHD) au Right Hand Drive (RHD)? Tanzania tunaendesha gari tukiwa tumekaa kulia kwa gari. Ukinunua gari ya RHD utapata shida sana kwenye kuovertake.

Maana ukitaka ku overtake katika njia ya magari mawili lazima uchungulie kama kuna gari inakuja mbele yako. Sasa fikiria ukiwa umekaa kushoto kwa gari na kuna gari nyingine mbele yako.

Kilometre gari lilizotembea

Hili nalo ni swala la msingi kumuuliza muuzaji wa gari na kutumia wauzaji waaminifu. Maana pia kuna ujanja wa wauzaji kucheza na kile kifa cha kutunza kumbuku kumbu ya Kilometre au umbali gari iliyotembea (Odometer).

Wauzaji wasio waaminifu wanauza magari chakavu sana kwa bei isiyostahili baada ya kuchakachua kilometre.

Kwa kawaida kwa magari ya binafsi jitahidi kununua gari chini ya Kilometre laki moja.

Bei ya gari, usafirishaji, insurance pamoja na ukaguzi

Baada ya kupitizia vigezo vyote na kuamua kuchagua gari, inabidi kuangalia gharama za usafirishaji mpaka bandari karibu na wewe, insurance pamoja gharamza ukaguzi jumla ni sh ngapi.

Inabidi kuhakikisha bei unayochagua ni Cost, Insurance and Freight (CIF). Bei ya CIF inajumusha gharama za manunuzi, insurance na usafirishaji wa gari mpaka bandari iliyo karibu na wewe.

Usichanganye bei ya CIF na bei ya Freight On Board (FOB). Bei ya FOB ni bei ya gari yako wakati ipo kwenye bandari ya muuzaji.

Bei ya FOB inajumuisha gharama za gari na gharama za kuipeleka gari bandarini na kuipakia kwenye meli tayari kwa safari.

Wauzaji wanapenda kuweka magari kwa bei hii ili yaonekane sio ghali. Ila zingatia kupata bei ya CIF. Ndo bei halisi utakayolipia.

Bandari gani ya kutumia utaamua wewe binafsi, ila hizi website tayari zina bandari wanazoweza peleka gari kwahiyo utachagua iliyo karibu na wewe.

Pia kuna gharama ya ukaguzi wa gari kama kuwa na hitilafu au tatizo lolote. Baada ya ukaguzi kuna cheti kinatolewa. Hichi cheti ni muhimu kwasababu kitahitajika wakati wa kulitoa gari lako bandarini.

kama huna hichi cheti itabidi kufanya ukaguzi Tanzania. Gharama za ukaguzi Tanzania ni kubwa ukilinganisha na za Japan. Hakikisha unafanya ukaguzi Japan.

Je gari ni manual au automatic gia, lina 4-Wheel Drive au lah

Ili pia ni swali la kujiuliza. Je unataka gari yenye gia manual au automatic?

Je unataka gari iwe na 4-wheel drive au lah?

Hatua #3: Gharama za viwango vya ushuru wa kutoa magari bandarini (MUHIMU)

Kabla hujalipia bei ya gharama (CIF) ni muhimu kupata makadirio ya kodi na ushuru utakaolipa bandarini ili kujua kiasi cha hela unachotakiwa kuandaa.

Mara kadhaa nimeona watu wanaagiza magari bila kujiandaa na ushuru na kodi utakayokuja kulipa bandarini gari lako likishafika.

Mwisho wa siku wanashindwa kuyatoa magari na baadae kuja kulipia hela nyingi zaidi kutoa gari kwa sababu ya gharama za utunzaji gari bandirini.

TRA wamerahisha tathimini ya kodi utakayolipa bandarini kwa kupitia TRA Tax calculator kwenye website yao.

Kwa mfano tukutumia specifications za Raum niliyoagizaga.

Jaza fomu ya TRA Valuation calculator kulingana na specifications za gari yako. Kwa mfano huu ntatumua specifications za Toyota Raum niliyoagizaga.

Ukishabonyeza Calculate utapata report kama ifuatavyo. Angalia kwa makini sehemu nilizozizungushia na red.

Customs Value CIF hii ni bei  elekezi  ya TRA wanakadiria thamani ya gari yako kulingana na uzoefu wao na taarifa walizonazo.

Muhimu: Kama gari lako likiwa na CIF tofauti na bei elekezi ya TRA kodi utakayolipa pia itabadilika. Na shauri uongee na clearing agent wako kwa ushauri wa kitaalamu au tuandikie.

Excise Duty due to Age hii ni kama kodi unalipa kwasababu ya uchakavu. Ukiagiza gari lililotengenezwa zaidi ya miaka kumi tangu leo, lazima uilipe hii.

Hatua #4: Jinsi ya kulipia gari

Ukishajiridisha na ubora wa gari na tathmini ya kodi na ushuru, unaweza kulipia kwa kutuma hela kwa muuzaji.

Ila inabidi ucheki na muuzaji kumuuliza tena kama gari uliyopipenda bado ipo sokoni na pia usisahau kuomba punguzo la bei. Sio mbaya kuuliza kama lipo.

Mara nyingi magari mazuri yenye bei poa yanauzika haraka, kwahiyo inabidi uwe mshapu kwenye kufaya maamuzi. Hili ni soko la magari used kwahiyo kila gari linakuwa lina utofauti na jingine.

Muuzaji atakupa taarifa zake za kibenki kwenye profoma invoice. Utaiprint hiyo invoice na kwenda nayo kwenye bank iliyokaribu nayo na kuwauliza utaratibu wa kutuma hela nje ya nchi kwa TT.

Ukishatuma hela, benki watakupa risiti na kukutaarifu lini hela zitaingia kwenye akaunti ya muuzaji, hii risiti utamtumia muuzaji ili aanze fwatilia malipo yako.

Hatua #5: Usafirishaji wa gari

Baada ya muuzaji kupokea hela yako, atasafirisha gari kulingana na muda mliokubaliana. Gari likashapikiwa kwenye meli, meli itampa muuzaji B/L document. Hii B/L document ndo utakayoitumia kutolea gari lako bandarini.

Muuzaji ataituma B/L document kwa DHL/Fedex na wewe inabidi shapu utakayopoipokea tu umkabidhi wakala wa kutoa mizigo bandarini kwa ajili ya kuanza mchakato wa kulitoa gari lako. Hii inabidi uipate kabla meli haijafika.

Gari yako ikifika bandarini inapata utunzaji wa bure kwa week moja,baada ya hapo unakuwa unalipia kwa kila siku gharama za utunzajia.

Kuepuka gharama za utunzaji wa gari bandarini. Inabidi uipate B/L document mapema na kumkabidhi wakala wa kutoa mizigo bandarini mapema na kumfwatilia kama ameshaanza mchakato wa kulitoa gari likiwasili.

Mara nyingi meli zinatumia week 3-4 hadi kutoka Japan hadi Tanzania. Kwahiyo mpaka meli ikifka unakuwa umeshaanza mchakato wa kutoa gari lako.

Hatua #5: Kupokea gari na kulipia kodi na ushuru

Gari lako likishafika, wakala wako wa kutoa mizigo bandarini atakutaarifu kuhusu gharama za kodi unayotakiwa kulipa, kumbuka tulijaribu kadiria gharama za kodi kwahiyo gharama zinaweza kuwa juu au chini kidogo.

Ukipokea gari lako likague kama kuna kitu chochote kimeibiwa nk. Maana mara nyingine vitu vinaibwa pale bandarini.

Jihadhari na aina mbalimbali za utapeli

Nimejaribu kukuelezea vitu muhimu vya kufanya wakati upo kwenye mchakato wa kuagiza gari. Ila matapeli pia nao wamekuwa wabunifu sana sana kwenye utapeli.

Mara nyingi matapeli wanatuma email, websites, account number zinazoendana na za wauzaji halali wa magari, kwa kutumia logo na maandishi yanayofanana. Kuwa makini sana.

Hitimisho

Nimejaribu kukuelezea kulingana na uwezo wangu jinsi ya kuagiza gari. Ila umakini unahitajika sana kuepukana na matapeli.

Ushauri wangu mshirikishe mtu mwenye uzoefu kama hauna uzoefu kabisa.

Wasiliana nasi tukusaidie agiza gari lako kwa usalama zaidi.

Una swali? Tuulize tukusaidie